HISTORIA FUPI YA MZEE AMBILIKILE MWANYALUKE PANJA ANAYESADIKIKA KUWA NA UMRI WA MIAKA 127
Imeandaliwa na mwandishi wetu.
Mzee Ambilikile Mwanyaluke Panja anayesadikika kuwa na umri wa miaka 127 anaishi katika kitongoji cha Izyika, Kijiji cha Majengo kata ya Ihanda umbali wa takriban Kilometa moja magharibi ya kituo cha mabasi cha Ihanda kilichopo barabara kuu inayotoka Afrika Kusini kwenda Cairo Misri.
Mzee Panja kutokana na hali ya afya yake inayotokana na umri mkubwa alionao bado ana kumbukumbu ya matukio makuu ya kwa mfano biashara ya utumwa iliyoratibiwa na Chifu Melele wa Tatu, vita vya maji maji, Vita ya kwanza na ya pili ya dunia ndani ya Kijiji cha Majengo.
Aidha, Mzee Ambilikile amepungukiwa uwezo wa kusikia kwani ahitaji sauti kubwa ili kuweza kusikia vizuri, anaweza kumtambua mtu kama atakuwa karibu naye. Mpaka sasa ni miaka mitatu mzee Panja anatumia kiti cha magurudumu kwa sababu hawezi kutembea kwa miguu yake.
Mzee huyo anapenda kutumia lugha yake ya asili ya Kindali ingawa anasikia Kiswahili.
Inasadikika kuwa Mzee Ambilikile Panja alizaliwa mwaka 1890 katika Kijiji cha Kapelekeshi kilicho katika Kata ya Kafule wilaya Ileje.
Mzee Panja anasema hajui mwaka aliozaliwa na kwamba wakati ule walikuwa hawana kumbukumbu za tarehe mpaka shule za mkoloni zilipoanzishwa. Hivyo makadilio ya umri wake yanatokana na kumbukumbu ya matukio aliyoyashuhudia na kusimuliwa.
Mzee Ambilikile anakumbuka kipindi cha utumwa ambacho kilifanywa na Chifu Melele wa Wasangu miaka ya mwanzoni mwa mwaka 1900 kupitia kwa wakala wake ambaye anamkumbuka kwa jina la Tuta. Panja anasema kipindi hicho walikuwa wanajificha pamoja na Wazazi wao kwenye mapango ya mawe milimani. Alisema “ Tulikuwa tunajificha kwenye mapango na Wazazi wetu na Tuta alikuwa anatumia wenyeji wake kutuitwa kwa lugha ya Kindali ili tutoke lakini tulikuwa tunazuiliwa na wazazi tusiitike na wao walikuwa wanaogopa kuingia ndani, basi tulikaa ndani mpaka tukihakikisha wameondoka ndipo tulikuwa tunarudi nyumbani” .
Panja anakumbuka hadithi ya vita vya maji maji, anasema kuwa walikuwa wanasimuliwa kuwa vita inapiganwa kusini kati ya Wazungu na Waafrika ambapo waliambiwa Waafrika wana dawa ya kugeuza risasi kuwa maji. Wakati huo mzee Panja anasema alikuwa na ufahamu ila alikuwa hajaanza kuchunga kuchunga Ng’ombe kwa sababu baba yake hakuwa nazo.
Mzee Panja anakumbuka vita kuu ya dunia ya kwanza na alioa katika kipindi hicho mwaka 1916 ingawa anasema alioa kwa kuchelewa akijilinganisha na vijana wa umri wake.
Ukifuatilia tafiti zilizofanyika na Wataalam wa Anthropolojia kwa mfano; Wilson, M. ( 1963) Good Company: A study of Nyakyusa Age – Villages. inaonesha kuwa Wanyakyusa walikuwa wanoa kuanzia umri wa miaka 25. Wanyakyusa na Wandali wanafanana mila na desturi kwa kiasi kikubwa ikiwa ni pamoja na makuzi ya watoto wao kuanzia kufundishwa wajibu kwa jinsi na umri.
Kwa hiyo kama alioa mwaka 1916 akiwa na umri wa miaka 26 inawezekana alizaliwa mwaka 1990.
Pamoja na hayo mzee panja alioa Mke wa Kwanza Mungajhoba Chufo ambaye alikuwa mke mdogo wa Chifu Mwambugha Musomba wa Kijiji cha Malangali, Ileje lakini ndoa hiyo haikuchukua muda mrefu kwa sababu ilikuwa ilichukuliwa kama ni uporaji kiasi cha kumfanya apate adhabu ya kulipa faini kwa kosa hilo, mzee Panja hakubahatika kupata mtoto na Mke huyo. Baadaye alimwoa Agness Mlawa mwishoni mwa mwaka 1996 na wakajaliwa kupata watoto Marko Ambilikile na Kilonati na baada ya hapo alioa wake wengine wawili na kuweza kuzaa jumla ya watoto 24 kati ya hao 8 wa Kike na 16 wa Kiume. Mzee Panja ana Wajukuu 112 , Vitukuu na Vilembwe.
Mwaka 2014 mtoto wake wa Pili kwa mke wa pili Agness Mlawa alikuwa anaitwa Kilonati Ambilikile Panja alifariki akiwa na umri wa miaka 98.
Aidha, alieleza kuwa kati ya watoto 24, ni watoto 11 tu walio hai mpaka anapotoa taarifa hiyo kwa msaada wa ukalimani wa mtoto wake Lawrance Ambilikile Panja Aprili 27,2017
2 Nselewa Mkoani RD, 54180 Mlowo-Mbozi
Anuani ya Posta: P.O.BOX 23 SONGWE
Simu: 025 2580305
Simu ya Kiganjani: 025 2580305
Barua pepe: ras@songwe.go.tz
Hakimiliki©2020 Mkoa wa Songwe.Haki Zote Zimehifadhiwa.