Naibu Waziri Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Juliana Daniel Shonza mapema leo ametoa vifaa mbalimbali vya michezo, Elimu na watu wenye Ulemavu vyenye thamani ya shilingi milioni 10,325,000 kwa Mkuu wa Mkoa wa Songwe.
Naibu Waziri Shonza ametoa Kompyuta Mbili, baiskeli mbili za watu wenye ulemavu, mipira na jezi kwa Brig. Jen. Nicodemus Mwangela huku akimpongeza kwa namna ambavyo amekuwa akiongoza jitihada mbalimbali za maendeleo ya Mkoa wa Songwe.
“Nimeona nami nije kuunga Mkono jitihada za Mkoa kama Naibu Waziri lakini pia mbunge wa Mkoa wa Songwe, tunaziona Jitihada za Mkuu wa Mkoa katika kukuza sekta mbalimbali, napenda kuwaambia huu ni mwanzo tu name nitaendelea kuleta vitu mbalimbali.”, amesema Naibu Waziri Shonza.
Aidha ameupongeza Uongozi wa Mkoa kwa kufanya maamuzi ya kununua timu ya Mpira wa Miguu itakayocheza ligi kuu ambayo itaweza kuuwakilisha Mkoa wa Songwe kitaifa na Kimataifa huku akiongeza kuwa Mkoa unafanya vizuri sana katika sekta ya Michezo.
“Mara ya Kwanza Mkoa wa Songwe kushiriki mashindano ya UMISETA ulishika namba moja katika Mpira wa Miguu nchi nzima na mara ya pili ulishika nafasi ya pili, hii ni ishara kuwa Songwe kuna vipaji vya kutosha.”, amesisitiza Naibu Waziri Shonza
Naibu Waziri Shonza amesisitiza kuwa jitihada hizi za kukuza sekta ya michezo ziendane na kutafuta uwanja ambapo ameshauri uongozi wa Mkoa kuhakikisha wanakuwa na uwanja wenye hati, uwe na uzio na usafishwe kisha maombi ya kujengewa uwanja yawasilishwe Shirikisho la Mpira wa Miguu Nchini (TFF).
Naye Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brig. Jen. Nicodemus Mwangela amempongeza Naibu Waziri Shonza kwa kukumbuka nyumbani na kuleta vifaa hivyo ambavyo vimegusa sekta Mbalimbali.
Brig. Jen. Mwangela amesema wananchi wanaonyesha kupenda michezo hususani katika kumiliki timu yao ya Mkoa hivyo wanaomba Wizara isaidie katika upatikanaji wa haraka wa uwanja pale watakapo kamilisha taratibu za awali zilizo elekezwa huku akiongeza kuwa vifaa alivyoleta vitaleta matunda mazuri katika sekta za michezo na elimu.
Katibu wa CCM Mkoa wa Songwe Mercy Mollel amempongeza Naibu Waziri Shonza kwa Kukumbuka nyumbani kwao na kuleta vifaa hivyo ambavyo vitawafanya vijana wajitume Zaidi hususani katika sekta ya michezo ili waweze kukumbukwa na kuletewa vifaa vingine zaidi.
Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Mlowo Grace Kashililika amemshukuru Naibu Waziri Shonza kwa kuipatia shule yake Kompyuta tano kwakuwa wamezoea kupewa ahadi na wanasiasa lakini wamekuwa hawatimiziwi ahadi zao tofauti na yeye.
Kashililika amesema sasa wataliomba Baraza la Mitihani Taifa ili mwakani wanafunzi wa shule yake waweze kufanya mitihani ya kompyuta kwa vitendo kwakuwa walishindwa kufanya hivyo kufuatia upungufu wa kompyuta.
Kwa upande wake Nuru Mwasasu mama mzazi wa Mtoto mwenye ulemavu Mary Mwakanyamale amemshukuru Naibu Waziri Sonza kwa kumpatia kiti kwa ajili ya mtoto wake huyo mwenye ulemavu.
Amesema sasa mtoto huyo mwenye umri wa miaka mtano lakini hawezi kukaa ataweza kukaa kwa kutumia kiti hicho na kumpunguzia kulala muda wote.
2 Nselewa Mkoani RD, 54180 Mlowo-Mbozi
Anuani ya Posta: P.O.BOX 23 SONGWE
Simu: 025 2580305
Simu ya Kiganjani: 025 2580305
Barua pepe: ras@songwe.go.tz
Hakimiliki©2020 Mkoa wa Songwe.Haki Zote Zimehifadhiwa.