RC KINDAMBA AAGIZA MIKAKATI YA KUDHIBITI KIPINDUPINDU KISITOKEE IIMARISHWE
SONGWE: Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Mhe. Waziri Kindamba amemuagiza Mganga Mkuu wa Mkoa pamoja na timu yake ya afya kuhakikisha wanajipanga vizuri kudhibiti ugonjwa wa kipindupindu kuingia Nchini ambao tayari umeripotiwa kuenea kwa sehemu kubwa na mamlaka za Nchi ya Malawi.
Mhe. Waziri Kindamba amewataka watalamu wa Afya kuimarisha mifumo yote ya Afya ikiwemo elimu kwa umma juu ya hatua za kuchukua ili kujiepusha na ugonjwa wa kipindupindu kuingia hapa nchini.
Mhe. Kindamba amesema ugonjwa wa kipindupindu ni hatari hivyo ni vyema kuzingatia usafi wa mazingira ili kuweza kuepuka ugonjwa kuingia Nchini.
Serikali haipendi kusikia ugonjwa huu umeingia nchini, nami sitaki kusikia hivyo, ukizingatia sasa tunaenda kwenye msimu wa mvua na Nchi jirani tayari ugonjwaa upo, ni wakati sasa timu za Afya ngazi ya Mkoa na Wilaya kuimarisha huduma mpakani ili kudhibiti ugonjwa huu, amesema Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Mhe. Waziri Kindamba.
Mganga Mkuu Mkoa wa Songwe Dkt. Boniface Kasululu amesema tayari timu ya watalamu wa Afya wameanza kutoa elimu kwa wananchi na viongozi wa vijiji vilivyopo mpakani juu ya kujikinga na kipindupindu ambao umeripotiwa nchini Malawi.
Pia, Dkt. Boniface Kasululu ametoa wito kwa wananchi kuhakikisha wanazingatia Kuchemsha maji ya kunywa au kuyatibu na dawa na kuyaweka sehemu salama, kujiepusha kuchafua vyanzo vya maji kwa kuoga au kufulia, kuepuka kula chakula kilichopoa au kinachoandaliwa katika Mazingira yasiyo safi na salama, kunawa mikono kwa maji tiririka kwa sabuni, kuosha matunda kabla ya kula ili waweze kujikinga na kipindupindu.
Aidha, Dkt. Kasululu ametoa wito kwa mwananchi ambaye atapata ugonjwa wa kutapika na kuharisha kufika mapema katika vituo vya kutolea huduma za Afya ili apatiwe matibabu haraka, kwani moja ya dalili za kipindupindu ni kuharisha na kutapika.
Bwn. Abu Zuberi Msemo Mkurugenzi wa mawasiliano kutoka kampuni ya Tanzania Communication and Development Center (TCDC) ameiomba Serikali kusaidia upatikanaji wa maji Safi sehemu za mikusanyiko kama shuleni, Sokoni na kuhakikisha sehemu izo wanatumia vyoo bora ili kujikinga.
MWISHO.
2 Nselewa Mkoani RD, 54180 Mlowo-Mbozi
Anuani ya Posta: P.O.BOX 23 SONGWE
Simu: 025 2580305
Simu ya Kiganjani: 025 2580305
Barua pepe: ras@songwe.go.tz
Hakimiliki©2020 Mkoa wa Songwe.Haki Zote Zimehifadhiwa.