Mkuu wa Mkoa wa Songwe Chiku Gallawa ameitaka Bodi Mpya ya Mamlaka ya Maji ya Vwawa-Mlowo aliyoizindua mapema leo, kusimamia upatikanaji wa maji safi na salama Mkoani hapa.
Gallawa ametoa rai hiyo nakuitaka bodi hiyo kuwa msimamizi wa huduma za maji huku akiitaka ijikite katika kubuni mbinu mbalimbali za kuboresha upatikanaji wa maji na utoaji wa huduma za maji kwa ufanisi.
“Bodi hii kwanza itusaidie kuongeza asilimia ya upatikanaji wa maji angalau tufikie asilimia 90 ifikapo mwaka 2020, pili ishirikiane na wadau kubuni mbinu mbalimbali za kuboresha huduma ya maji, lakini pia isimamie utunzaji wa vyanzo vya maji”, amesisitiza Gallawa.
Ameongeza kuwa bodi hiyo ijiendeshe kidijitali kwa kuweka mfumo wa kutuma bili za maji kwa mfumo wa ujumbe mfupi na kusisitiza kuwa wateja wawekewe mita na bili zao ziwe halisi sawasawa na matumizi yao.
Gallawa amesema, “Tumepiga vita biashara ya mkaa ili kutunza mazingira, bodi ihakikishe sasa vyanzo vyote vya maji vinalindwa pia iweke mikakati ya uvunaji wa maji ya mvua kwa mabwawa na hata kwa majumbani na pia mkakati mwingine uwe wa kuhakikisha maji yanayopatikana yanakuwa safi na salama”.
Amewahakikishia wajumbe kuwa ana imani na utendaji wao huku akiwataka kushirikiana na halmashauri katika kuthibiti taka ngumu kwakuwa zinaweza kuchafua vyanzo vya maji hivyo kuleta magonjwa ya mlipuko.
Aidha amewatahadharisha kusimamia vema mapato yatakayokusanywa, fedha za wadau na fedha kutoka serikalini ili mamlaka iweze kusimama imara pia wasimamie miradi ya maji inayojengwa ikamilike kwa muda na kwa ubora unaotakiwa.
Naye Mwenyekiti wa Bodi hiyo Asanga Malalwale Ndile ameshukuru Mkuu wa Mkoa wa Kuzindua bodi hiyo pamoja ushirikiano ambao amekuwa akiwapatia wakat wa uundwaji wake.
Ndile amesema atahakikisha anashirikiana na wajumbe, wadau na serikali katika kuhakikisha sekta ya maji Mkoa wa Songwe inaboreshwa huku akiwa na imani kuwa bodi hiyo itafanya vizuri kiutendaji licha ya upya wake.
Kwa upande wake Mhandisi wa Maji Mkoa wa Songwe Tanu Deule ameeleza kuwa hali ya upatikanaji wa maji kwa Mkoa wa Songwe ni asilimia 42.5 ambapo matarajio ni kuwa ifikapo Juni 2018 hali ya upatikanaji wa maji itakuwa ni asilimia 59.61.
Deuli ameongeza kuwa asilimia hiyo ya maji itaongezeka mara tu baada ya kukamilika kwa miradi zaidi ya kumi ya maji iliyopo kwenye bajeti ya mwaka 2017/18.
Mhandisi wa Maji Mkoa wa Songwe Tanu Deule akisoma taarifa ya hali ya upatikanaji wa maji wakati wa uzinduzi wa bodi ya Mamlaka ya Maji ya Vwawa-Mlowo.
2 Nselewa Mkoani RD, 54180 Mlowo-Mbozi
Anuani ya Posta: P.O.BOX 23 SONGWE
Simu: 025 2580305
Simu ya Kiganjani: 025 2580305
Barua pepe: ras@songwe.go.tz
Hakimiliki©2020 Mkoa wa Songwe.Haki Zote Zimehifadhiwa.