Mkuu wa Mkoa wa Songwe,Mhe. Dkt. Francis K. Michael, ameipongeza serikali ya Awamu ya Sita Chini ya Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kutenga TZS 200 Milioni kusaidia sekta ya kilimo kufanikisha utafiti wa zao la Pareto kupitia Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI) Kituo cha Uyole. Dkt. Michael ameonesha furaha yake kuhusu hatua hii muhimu, hasa kwa kuinua sekta ya kilimo, ikiwemo zao la Pareto ambalo kwa muda fulani lilisahaulika. Amesisitiza kuwa Mkoa wa Songwe una uwezo mkubwa wa kuzalisha tani 12,000 za maua makavu ya Pareto, na hii ni fursa kubwa ya kuboresha uchumi wa Mkoa wa Songwe
Katika kufanikisha jitihada hizi, Kituo cha Utafiti wa Mazao ya Kilimo TARI Kituo cha Uyole kimefanya utafiti wa mbegu za Pareto. Mkurugenzi wa Bodi ya Pareto nchini, Lucas Ayo, alisema kuwa serikali imetoa TZS 200 Milioni kwa ajili ya utafiti zaidi katika zao hilo. Utafiti huu unatarajiwa kuboresha ubora na uzalishaji wa Pareto nchini.
Kwa kuzingatia umuhimu wa kuongeza uzalishaji wa zao la Pareto nchini Tanzania, serikali imetangaza mpango wa kutoa kilo 2,000 za mbegu za Pareto bure kwa wakulima katika nchi nzima. Katika jitihada za kuimarisha uzalishaji wa zao hili, Mkoa wa Songwe, na hasa Wilaya ya Ileje, umepokea gawio la kilo 260 za mbegu hizi. Hatua hii inatarajiwa kusaidia kuongeza uzalishaji wa Pareto na kufikia lengo la kuzalisha tani 1,000 za maua makavu ya Pareto kwa msimu mmoja.
Ni muhimu kutambua kuwa Tanzania ni nchi pekee katika bara la Afrika inayolima Pareto, na ni nchi ya pili duniani kwa uzalishaji wa zao hili. Zaidi ya hayo, Tanzania inajulikana kwa kuzalisha Pareto yenye ubora wa hali ya juu, na uzalishaji wake kuu unafanyika katika mikoa ya nyanda za juu kusini. Hii ni habari njema kwa wakulima na wafanya biashara katika kukuza uchumi wa mkulima na taifa kwa ujumla kupitia sekta ya kilimo .
2 Nselewa Mkoani RD, 54180 Mlowo-Mbozi
Anuani ya Posta: P.O.BOX 23 SONGWE
Simu: 025 2580305
Simu ya Kiganjani: 025 2580305
Barua pepe: ras@songwe.go.tz
Hakimiliki©2020 Mkoa wa Songwe.Haki Zote Zimehifadhiwa.