SERIKALI KUPIMA UPYA ENEO LA NANYALA KUONDOA MGOGORO.
MBOZI: Serikali Mkoani Songwe imesema ina mpango wa kuligawa eneo la zaidi ya ekari 1,800 lenye hati namba 31 lililopo Kijiji cha Nanyala ambalo kwa muda mrefu limekuwa na mgogoro kati ya Kwanda cha Saruji cha Mbeya, wananchi wa Kijiji cha Nanyala pamoja na wadau wengine ambao wanafanya shughuli za uchimbaji madini katika kijiji hicho.
Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Mhe. Omary Mgumba amesema hayo wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika Aprili 8, 2022 na wananchi wa Kijiji cha Nanyala, Mbeya cement pamoja na wadau wanaofanya shughuli za uchimbaji katika Kijiji cha Nanyala.
Mhe. Mgumba amesema timu ya wataalamu iliyoundwa na Rais wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan itapita kubaini maeneo yanayofaa kwa Kiwanda cha Mbeya Cement, kwa Kilimo, madini ya chokaa, marble na eneo la wananchi ili kila mtu abaki na eneo ambalo linafaa kwake kwa shughuli za kiuchumi.
Amesema kuna mgogoro kwa sababu Serikali ilitoa hati ya miaka 99 ya kiwanja namba 31 kwa kiwanda cha Mbeya cement, wakati wapo wananchi wanaomiliki kisheria na wana hati za kimila, kuna wengine wameachiwa na babu zao pia kuna wadau wanafanya shughuli za uchimbaji wa madini na wamepewa leseni halali na Serikali ya Tanzania.
"Kiwanda cha Mbeya Cement kimeondoa kesi Mahakamani baada ya kuona hakuna masilahi ya kuendelea na kesi Mahakamani wakati wana uwezo wa kumaliza mgogoro huo kwa pamoja kati ya Mbeya Cement, wananchi wa Nanyala, wadau wanaofanya shughuli za uchimbaji na Serikali" Omary Mgumba.
Diwani wa Kata ya Nanyala, Mhe. George Musyani ameishukuru Serikali kuja na mpango wa kupima upya ardhi kwani ndani ya ekari 1,800 ambazo Mbeya Cement wanadai ni za kwao na wananchi wa Nanyala wanalitegemea kiuchumi kwani wana mashamba yao, migodi na baadhi ya vitongoji vipo umo kama cha Majimoto, Iwanga, Udinde, Malema ambayo kuna miundombinu ya huduma za jamii.
Naye Julius Mwashilindi mwananchi wa Kijiji cha Nanyala amesema kitendo cha Mbeya Cement kuamua kumiliki ardhi bila ya kuwa na mkutano wa hadhara na kijiji ndio chanzo kikubwa cha mgogoro.
Aneth Gambi Mkazi wa Nanyala amesema ardhi ya Nanyala ni mali yao ambayo vizazi kwa vizazi vimeishi pale na wameiomba Serikali kutenda Haki.
Ikumbukwe kwa mara kadhaa wananchi wa Kijiji cha Nanyala wamelalamika kero yao hii kwa Waziri Mkuu pamoja na Rais wa Tanzania wa awamu ya 5 Mhe. Hayati John Magufuli alipofanya ziara 2019 Songwe na kuongea na wananchi wa Kijiji cha Nanyala.
MWISHO.
2 Nselewa Mkoani RD, 54180 Mlowo-Mbozi
Anuani ya Posta: P.O.BOX 23 SONGWE
Simu: 025 2580305
Simu ya Kiganjani: 025 2580305
Barua pepe: ras@songwe.go.tz
Hakimiliki©2020 Mkoa wa Songwe.Haki Zote Zimehifadhiwa.