SERIKALI KUSHIRIKIANA NA TAASISI ZA DINI KUTATUA CHANGAMOTO
Na. Nicholaus Ndabila
SONGWE: Mkuu wa Mkoa wa Songwe Mhe. Waziri Kindamba amesema Serikali itashirikiana na Taasisi za dini zote katika kutatua changamoto zilizopo ndani ya Mkoa wa Songwe.Mkuu wa Mkoa wa Songwe amesema hayo Agosti 4 alipowatembelea vongozi wa Parokia ya mtakatifu Patrick Vwawa pamoja na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) kwa lengo la kujitambulisha kwa viongozi hao baada ya kuteuliwa na Rais wa Tanzania, Mhe. Samia Suluh Hassan kuwa Mkuu wa Mkoa wa Songwe.
Mkuu wa Mkoa amesema wakati Serikali inapita mitaani kuhakikisha ulinzi na usalama unakuwepo, viongozi wa dini wao wanasaidia kuweka amani kwenye mioyo ya watu kwani binadamu ni kiumbe mgumu sana akiachwa bila kupewa nasaha za kutosha basi amani na utulivu unakuwa mashakani.
“Kuna msemo unasema ukitaka kufanikiwa waweke viongozi wa dini karibu na ukitaka kufeli basi waweke viongozi wa dini mbali, Serikali tumechagua kuwaweka karibu viongozi wa Dini” Mhe. Waziri Kindamba.
Aidha, Mkuu wa Mkoa wa Songwe ameomba ushirikiano kwa Taasisi za kidini kusaidia Serikali kutoa elimu kwa waumini wao juu ya kushiriki katika zoezi la SENSA ya watu litakalofanyika Agosti 23 pamoja kupata na kuhamasisha wananchi wapate chanjo ya UVIKO 19.
Mchungaji John Mwasakilali wa KKKT amempongeza Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Mhe. Waziri Kindamba kwa kuaminiwa tena na Rais wa Tanzania na kuletwa kwenye Mkoa ambao una mahitaji makubwa ya kimiundombinu na changamoto ili aweze kuzitatua.
Pia, Mch. Mwasakilali amemueleza changamoto kadhaa Mkuu wa Mkoa ambazo amemuomba kuzitafutia majawabu ikiwemo upungufu wa nishati ya kupikia katika mji wa Vwawa kama vile mkaa, kuni na bei kubwa ya gesi ya kupikia pamoja na upungufu wa maji katika mji wa Vwawa.
Wakati huo huo, Mkuu wa Mkoa amewaomba viongozi wa dini kutochoka kuishauri Serikali mara kwa mara ili kuweza kutatua changamoto kwa pamoja za wananchi na amewakaribisha ofisini kwake muda wowote watakapohitaji kufika.
MWISHO.
2 Nselewa Mkoani RD, 54180 Mlowo-Mbozi
Anuani ya Posta: P.O.BOX 23 SONGWE
Simu: 025 2580305
Simu ya Kiganjani: 025 2580305
Barua pepe: ras@songwe.go.tz
Hakimiliki©2020 Mkoa wa Songwe.Haki Zote Zimehifadhiwa.