Siku ya Kilele cha Maadhimisho ya Elimu ya Watu Wazima kwa mara ya kwanza Mkoa wa Songwe yamefanyika katika Wilaya ya Mbozi, mji wa Vwawa katika Shule ya Msingi Mwenge. Maadhimisho haya yalifuata maelekezo ya serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambayo yanasisitiza umuhimu wa kuinua elimu ya watu wazima, hususan kwa wasichana ambao wamekutana na changamoto mbalimbali zinazowazuia kuendelea na masomo.
Hafla hii ilikusanya viongozi mbalimbali, akiwemo Mkufunzi Mkazi wa Mkoa, Kaimu Mkurugenzi wa Wilaya ya Mbozi, wakuu wa idara za elimu ya msingi na sekondari, na maafisa elimu ya watu wazima kutoka Mkoa wa Songwe. Pia, walimu wa shule za msingi na sekondari, pamoja na wanafunzi wa elimu ya watu wazima kutoka kituo cha Iposa, walishiriki kikamilifu katika maadhimisho haya yenye umuhimu wa kipekee.
Mgeni Rasmi wa hafla hii alikuwa Mwl. Hance Mgaya, Afisa Taaluma wa Mkoa. Aliitumia fursa hii kuishukuru Halmashauri ya Mbozi kwa kuandaa maadhimisho haya ya kihistoria katika Mkoa wa Songwe. Vilevile, alimpongeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi na wote walioshiriki katika kuandaa maadhimisho haya. Alisisitiza umuhimu wa halmashauri zingine katika Mkoa wa Songwe kujiandaa mapema kwa ajili ya maadhimisho ya mwaka ujao ili yafanyike kwa ufanisi mkubwa zaidi.
Katika hotuba yake, Mgeni Rasmi alielezea umuhimu wa elimu ya watu wazima katika kupambana na ujinga, umaskini, na magonjwa ya kawaida ulimwenguni. Alifafanua kuwa Juma la Elimu ya Watu Wazima Duniani husherehekewa kuanzia tarehe 01/09 hadi tarehe 08/09 kila mwaka, na kwamba maadhimisho haya yanafuatilia ratiba ya matukio ya kitaifa kama vile sensa, mbio za mwenge wa uhuru, uchaguzi mkuu, na mitihani ya kuhitimu elimu ya msingi.
Mwl. Hance Mgaya pia alisisitiza kuwa shule zote za msingi na sekondari zinaweza kutumika kama vituo vya elimu ya watu wazima. Elimu hii inawapa nafasi watu kujiendeleza kutoka viwango vya chini kabisa vya elimu hadi ngazi za juu kupitia programu mbalimbali kama mpango wa elimu ya msingi kwa walioikosa na mpango wa serikali wa njia mbadala (ASEP) ambao unalenga wasichana walioacha shule na wavulana ambao pia wamekatisha masomo.
Mgeni Rasmi alipata fursa ya kutembelea vyumba vya maonyesho na kushuhudia kazi nzuri inayofanywa na vijana wa kituo cha elimu ya watu wazima cha Iposa. Aliwapongeza kwa juhudi zao na kuwahimiza kuendelea kuongeza bidii katika kazi zao ili kuboresha ubora wa bidhaa zao, kuwa na ushindani katika soko, na kudumisha dhamira ya kujifunza kila siku, kwani hii ndiyo nguzo ya elimu ya watu wazima.
2 Nselewa Mkoani RD, 54180 Mlowo-Mbozi
Anuani ya Posta: P.O.BOX 23 SONGWE
Simu: 025 2580305
Simu ya Kiganjani: 025 2580305
Barua pepe: ras@songwe.go.tz
Hakimiliki©2020 Mkoa wa Songwe.Haki Zote Zimehifadhiwa.