Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brigedia Jenerali Nicodemus Mwangela ameutaka Uongozi wa Wilaya ya Songwe Kuongeza jitihada na nguvu Zaidi katika kukamilisha ujenzi wa Vituo vya Afya vya Magamba na Mbuyuni pamoja na ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya hiyo.
Brigedia Jenerali Mwangela ameyasema hayo leo mara baada ya kupokea taarifa ya mpango wa ukamilishaji wa miradi hiyo kutoka kwa uongozi wa Wilaya ya Songwe na kisha kuwapeleka katika Mradi uliokamilika wa Kituo cha Afya ya Isansa Wilaya ya Mbozi na ujenzi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa ili waweze kujifunza kwa vitendo.
“Baada ya kupokea taarifa yao ya ukamilishaji wa miradi ya ujenzi ya Wilaya ya Songwe, nimeona ni vema waje wajifunze kwa vitendo kwakuwa ukamilishaji wa miradi yao ya ujenzi umekuwa ukienda taratibu mno pia wajifunze kufanya kazi za serikali kwa teamwork”, amesisitiza Brigedia Mwangela.
Brigedia Jenerali Mwangela amesema miradi ya ujenzi ya Wilayani humo mingi bado haijakamilika na muda umewaishia hivyo kwa ziara hiyo wajifunze kuwa wenzao wamekalisha miradi hiyo na inahudumia wananchi na pia kazi za serikali zinapaswa kukamilika kwa muda.
“Wao vituo vimechelewa sana kukamilika wamekuja wajifunze na waongeze nguvu ili waweze kukamilisha mapema, wameniambia wamejifunza kitu lakini pia wanapaswa kutambua kuwa kazi za serikali unapewa fedha, vifaa na muda maalumu wa kukamilisha”, ameeleza Brigedia Mwangela
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Songwe Samuel Jeremia Opulukwa amesema wamejifunza kuwa wenzao wameweza kumalizia ujenzi wa Vituo vya Afya kwa viwango vizuri na wao watafanya hivyo ili wananchi waanze kupata huduma.
“Tumeona wenzetu wamekamilisha vizuri nasi tutajitahidi kukamilisha vizuri vituo vyetu ya Afya vya Magamba na Mbuyuni pamoja na hospitali ya Wilaya ili tuweze kutoa huduma kwa wananchi wetu ifikapo Julai 30, 2019”, amesema Opulukwa.
Naye Mganga Mkuu wa Wilaya ya Songwe Humphrey Masuki amesema wamejionea namna nzuri ya umaliziaji wa vituo vya Afya ili viwe na ubora na kutoa mfano kuwa wamejifunza namna nzuri ya upangaji makabati katika chumba cha kuhifadhi maiti na upangaji wa makabati na meza katika jengo la maabara.
2 Nselewa Mkoani RD, 54180 Mlowo-Mbozi
Anuani ya Posta: P.O.BOX 23 SONGWE
Simu: 025 2580305
Simu ya Kiganjani: 025 2580305
Barua pepe: ras@songwe.go.tz
Hakimiliki©2020 Mkoa wa Songwe.Haki Zote Zimehifadhiwa.