Mkoa wa Songwe umefanikiwa kupunguza vifo vya akina mama wajawazito kutokana na ongezeko la vituo vinavyotoa huduma ya mama na motto kutoka 156 mwaka 2018 hadi kufikia vituo 185 kwa mwaka 2021 ikiwa ni pamoja na vituo vya Afya 7 vilivyoanza kutoa huduma ya upasuaji.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Dkt. Hamad Nyembea amesema 2018 kulikuwa na vifo 32, 2019 vifo 31, 2020 vifo 23 na 2021 kwa robo ya Januari na Machi vifo vitano tu.
Dkt. Nyembea ameongeza kuwa kwa kipindi cha Januari hadi Machi ya kila mwaka kutoka 2018-2021, Mkoa umezidi kupunguza vifo ikiwa 2018 kulikuwa na vifo 12, 2019 vifo 13, 2020 vifo 10 na kwa mwaka 2021 vifo 5 tu ikiwa ni mafanikio ya 50% na katika Halmashauri ya Wilaya ya Ileje hakukuwa na kifo hata kimoja.
Dkt. Nyembea amesema lengo la Mkoa ni kupunguza vifo vinavyozuilika vya mama mjamzito kwani asilimia 95 ya vifo vyote vinavyotokea vinaweza kuzuilika na watalamu kukiwa na miundombinu bora kwani sababu nyingi za vifo huwa ni nyepesi sana.
Pia, Dkt. Nyembea ameeleza sababu za vifo kwa wajawazito kuwa ni kuvuja damu nyingi ukeni, kifafa cha mimba, upungufu wa damu, kuchelewa kuanza kliniki na matatizo mengine.
Mkuu wa Wilaya ya Ileje, Joseph Mkude ameeleza sababu kubwa iliyopelekea Wilaya hiyo kutokuwa na kifo chochote cha mama mjamzito kwa kipindi cha miezi 4 ni kutokana na Kamati ya Usalama Wilaya hiyo kushiriki katika mapambano ya kutokomeza vifo vya akina mama kwa kuiweka kama agenda ya kudumu ya Kamati ya Usalama.
Pia, Mkude amesema ofisi ya Mganga Mkuu ilimshirikisha vizuri na waliweza kuzunguka vituo vyote kufanya ukaguzi wa kuhakikisha kuwa vifaa tiba na Dawa zote muhimu vinakuwepo kwenye vituo vyote.
"Baada ya kuzunguka vituo vyote Kamati ya Usalama tulianza kufuatilia mapungufu yote na kutoa maagizo nadhani ndio sababu kwa sasa Ileje hakuna kifo cha mama mjamzito.”, amesema Mkude.
Naye Mratibu wa Afya ya Uzazi na Mtoto Mkoa wa Songwe, Eva Mwakyusa amesema sababu nyingine iliyopelekea Songwe kupunguza vifo ni kutoa ushauri wa kitalamu pamoja na kutoa mafunzo kazini ya jinsi ya kukabiliana na dharura ya uzazi kwa vituo vinavyotoa huduma hizo.
2 Nselewa Mkoani RD, 54180 Mlowo-Mbozi
Anuani ya Posta: P.O.BOX 23 SONGWE
Simu: 025 2580305
Simu ya Kiganjani: 025 2580305
Barua pepe: ras@songwe.go.tz
Hakimiliki©2020 Mkoa wa Songwe.Haki Zote Zimehifadhiwa.