Wananchi wa Mkoa wa Songwe mna tahadharishwa juu ya uwepo wa ugonjwa wa Ebola uliotokea nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) katika jimbo la Kivu na kuenea mpaka katika jimbo la Ituri kuanzia Agosti 1, 2018.
Mpaka kufikia tarehe 15 Agosti, 2018 wagonjwa waliogundulika kuwa na virusi vya Ebola nchini DRC walikuwa 51, wanaohisiwa 27 huku waliofariki wakiwa 44, kwa wastani kati ya watu 10 waliopata Ebola, watu 5 hadi 9 hufariki.
Tahadhari hii inatolewa kwasababu eneo la mpaka wa Tunduma hutumiwa na raia wa Congo kuingilia nchini Tanzania kupitia nchi jirani ya Zambia na hivyo ugonjwa huu kuwa hatarini kuingia nchini Tanzania licha ya kuwa Mkoa wa Songwe haujapakana na nchi ya DRC moja kwa moja.
Serikali ya Mkoa kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imeweka hali ya tahadhari na kuchukua hatua muhimu ili kuhakikisha ugonjwa huu hauingii nchini, naendapo utaingia uweze kuthibitiwa mapema.
Baadhi ya hatua zilizochukuliwa ni pamoja na kuwekwa huduma za uchunguzi eneo la Mpaka wa Tunduma, huduma za kulazwa na mahali pa maziko endapo watabainika wagonjwa wa Ebola na wengine kufariki.
Aidha mafunzo kwa watoa huduma za Afya yalitolewa, vifaa tiba/kinga na dawa vilinunuliwa na Mkoa unaendelea kufanya ufuatiliaji huku huduma ya uchunguzi kwa abiria wanaotumia mpaka wa Tunduma zikiendelea.
Virusi vya Ebola havienei kwa njia ya hewa bali huambukiza kwa njia Kuu Mbili, ambazo ni Kutoka kwa Wanyama kwenda kwa Watu (endapo utamgusa mnyama mwenye Ebola au kula nyama yake) na Kutoka kwa mtu mwenye Virusi vya Ebola kwenda kwa mtu mwingine (kwa kugusana, kugusa majimaji ya mwili au damu).
Dalili za kwanza za Ugonjwa wa Ebola zinafanana na za magonjwa mengine ambazo ni homa ya gafla, uchovu, maumivu ya koo, tumbo, misuli, kichwa na viungo vingine. Kwa dalili hizo, watu hufikiria kwamba wana magonjwa mengine kama vile malaria au homa ya matumbo.
Kwa kawaida hali inayofuata ni kichefuchefu na kuharisha pamoja na figo kutofanya kazi vizuri, huku wengine huanza kutokwa na damu kwenye matundu yote ya mwili kama pua, masikio, mdomoni na sehemu ya haja kubwa.
Wananchi mtambue ya kuwa mpaka sasa hakuna mgonjwa wa Ebola aliyegunduliwa nchini Tanzania, na mpaka sasa hakuna tiba maalumu ya ugonjwa wa Ebola isipokuwa mtu akipata huduma bora mapema kutoka kwa madaktari na wauguzi mara baada ya kugunduliwa na ugonjwa huu anaweza kuishi.
Pia kama kuna mtu ana dalili zilizotajwa hapo juu na ana historia ya kutembelea nchi jirani ya Congo, apelekwe haraka kituo cha tiba ili afanyiwe uchunguzi mapema.
Imetolewa Na;
Grace Gwamagobe
Afisa Habari
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Songwe
18 Agosti, 2018.
Kwa taarifa Zaidi tembelea tovuti ya mkoa wa Songwe www.songwe.go.tz katika kipengele cha matangazo.
2 Nselewa Mkoani RD, 54180 Mlowo-Mbozi
Anuani ya Posta: P.O.BOX 23 SONGWE
Simu: 025 2580305
Simu ya Kiganjani: 025 2580305
Barua pepe: ras@songwe.go.tz
Hakimiliki©2020 Mkoa wa Songwe.Haki Zote Zimehifadhiwa.