Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brig. Jen. (Mst) Nicodemus Mwangela amewataka wananchi wa Vijiji vya Itewe, Sasenga na Mboji Wilayani Mbozi kurejea katika Mazungumzo na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kufuatia Mgogoro wa mipaka ya ardhi.
Brig. Jen. (Mst) Mwangela ameyasema hayo alipotembelea vijiji hivyo akiambatana na uongozi wa Kambi ya Jeshi ya Kikosi cha KJ 845 ambao wamekuwa kwenye mgogoro wa mipaka na vijiji hivyo tangu mwaka 1979.
Amesema kuwa eneo ambalo linatambulika rasmi kuwa linamilikiwa na Jeshi lina ukubwa wa hekta 1398 na hivyo mwananchi yoyote hataruhusiwa kumiliki eneo hilo na endapo yupo ambaye anaishi katika eneo hilo atoke, aidha Jeshi liliomba eneo lingine ambalo ndilo lina mgogoro.
“Tunarudi kwenye mazungumzo, Jeshi na vijiji vyote vya Itewe, Sasenga na Mboji, ninacho waomba, kila upande ulete uthibitisho wa umiliki wa eneo lake, mkisha wasilisha hati zenu au hata vithibitisho vya umiliki wa maeneo yenu tutakaa tujadiliane ili mgogoro huu uishe kwa amani”, amesisitiza Brig. Jen. (Mst) Mwangela
Aidha Brig. Jen. (Mst) Mwangela amewataka wananchi wa vijiji vyenye Mgogoro na Jeshi kuendeleza amani na kukubali kumaliza mgogoro huo kwa njia ya majadiliano, pia watambue kuwa Jeshi lipo kwa ajili ya wananchi hao.
“Mimi sitaegemea upande wowote katika mgogoro huu kwani natambua wananchi ni muhimu na jeshi pia ni taasisi ambayo ni muhimu Mkoani Kwetu kwa ajili ya ulinzi na usalama wetu, hivyo basi itakapo bainika jeshi linahitaji eneo zaidi basi wananchi wenzangu tuwafikirie hawa lakini pia tutahakikisha wananchi wanaondoka kwa utaratibu mzuri”, ameongeza Brig. Jen. (Mst) Mwangela.
Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Sasenga Yaledy Hassan Wegga amesema wananchi wako tayari kutoa eneo kwa Jeshi endapo utaratibu mzuri utafuatwa kwani wanatambua umuhimu wa Jeshi kwa ajili ya ulinzi na usalama wa raia na mali zao.
2 Nselewa Mkoani RD, 54180 Mlowo-Mbozi
Anuani ya Posta: P.O.BOX 23 SONGWE
Simu: 025 2580305
Simu ya Kiganjani: 025 2580305
Barua pepe: ras@songwe.go.tz
Hakimiliki©2020 Mkoa wa Songwe.Haki Zote Zimehifadhiwa.