UKOSEFU WA DAMU SALAMA, UWAJIBIKAJI WA WATALAMU SABABU YA VIFO VYA MAMA MJAMZITO
SONGWE: Mganga Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Dkt. Boniphace Kasululu amewataka waganga wafawidhi wa vituo vyote vinavyotoa huduma ya upasuaji kwa kushirikiana na waganga wakuu wa Halmashauri kuhakikisha damu salama inapatikana kwenye vituo vyao muda wote saa 24 ili kuwa tayari kwa dharura itakayojitokeza kwa mama mjamzito atakapohitaji damu salama.
Dkt. Boniphace Kasululu amesema hayo wakati kikao kazi cha robo cha kupitia taarifa za vifo vya uzazi vilivyotokea na sababu zake na kuweka mikakati ya kupambana na vifo hivyo kilichofanyika wilayani Ileje 10 Agosti 2022.
Dkt. Boniphace Kasululu amesema Mkoa wa Songwe umekuwa ukijitahidi kuhakikisha unapunguza vifo vya uzazi na watoto wachanga kuanzia umri 0 hadi siku 7 lakini bado changamoto ya vifo ipo na asilimia 95 ya vifo hivyo vingeweza kuzuilika kama watalamu wangezingatia maadili yao ya taaluma na uwajibikaji kazini na kuwa nia thabiti ya kuokoa maisha ya mama mjamzito na watoto wachanaga.
Dkt. Kasululu amesema akina mama wajawazito waliofariki mwaka 2019 walikuwa 31 sawa na vizazi hai 73/100,000 mwaka 2020 vifo vilikuwa 23 sawa na vizazi hai 53/100,000, mwaka 2021 vifo 28 sawa na vizazi hai 62/100,000 na kuanzia mwezi Aprili hadi Juni 2022 vifo viko 9 hali si nzuri sana inahitaji jitihada za makusudi kutatua tatizo ili.
Kwa watoto wachanga wa umri kuanzia 0 hadi siku 7 pamoja na wale wanaozaliwa wakiwa wamefariki kwa mwaka 2019 watoto 549 walifariki, 2020 watoto 515 walifariki, 2021 watoto 468 na kwa 2022 kuanzia mwezi wa kwanza hadi sita watoto 204, amesema Dkt. Boniphace Kasululu.
Mganga Mkuu wa Mkoa, Dkt. Boniphace Kasululu amesema vifo vingi vilivyotokea ndani ya mkoa wa Songwe vinaonyesha mama alikuwa anapoteza damu nyingi wakati anajifungua lakini unakuta kituo hakina damu salama, wakati watalamu wanajua kabisa sababu za vifo vingi vya uzazi ni ukosefu wa damu salama mama anapokuwa anajifungua.
”Mganga mwenye nia thabiti ya kuokoa maisha ya mama mjamzito hawezi kwenda kulala wakati Kituo chake hakina damu salama, akina maji, uku akijua kabisa kituo chake kinatoa huduma ya dharura na ukosefu wa damu salama ni chanzo cha kifo” Dkt. Boniphace kasululu.
Pia, Dkt. Boniphace Kasululu amewaagiza waganga wakuu wa Halmashauri kukusanya damu mara kwa mara kwa watu ambao wako tayari ili kuwa na akiba ya kutosha ya damu kwa ajili ya huduma za dharura kwa mama mjamzito.
Aidha, Mganga Mkuu wa Mkoa ametoa wito kwa wananchi kujitokeza kuchangia damu salama kwa ajili ya kuokoa maisha ya mama mjamzito wakati akijifungua, kwani takwimu zinaonyesha kwa miaka mitatu mfululizo Mkoa wa Songwe unashika nafasi ya mwisho kwa uchangiaji wa damu salama kitaifa.
Kitendo cha Mkoa wa Songwe kushika nafasi ya mwisho kwa uchangiaji damu ni ishara kama wananchi wa Songwe bado kukosa nia thabiti ya kupamba na vifo vinavyotokana na uzazi uku wakijua vifo vingi vinasabbishwa na upungufu wa damu.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Songwe, Bi. Happiness Seneda amesema yeye kama mama anaumia sana pale anaposikia kuna mwanamke amefariki kwa ajili ya uzazi, hivyo amemuagiza Mganga Mkuu wa Mkoa kuhakikisha anaweka mikakati thabiti ya kukomesha vifo vya mama mjamzito na mtoto.
Katibu Tawala amemtaka Mganga Mkuu wa Mkoa kuhakikisha kila kituo kinachotoa huduma ya dharura (kinafanya upasuaji) kiwe na watalamu wote wanaotakiwa kama vile mtalamu wa kutoa dawa ya usingizi, daktari wa kutosha pamoja na uwepo wa vifaa tiba vyote vya kisasa na viwe vinafanya kazi.
Pia, Katibu Tawala wa Mkoa wa Songwe, Bi. Happiness Seneda ameitaka Idara ya afya kuwa na utaratibu wa kuwaongezea ujuzi watalamu wake kama vile kuwapeleka shule ili kupata watalamu wengi zaidi ambao watakuwa kwenye vituo vya dharura na kuhakikisha hakuna vifo vya uzembe wa binadamu vinatokea.
Kwa mujibu wa tafiti za kitalamu, asilimia 85 ya akina mama wajawazito wanajifungua salama bila shida yeyote, mama anaweza kujifungua sehemu yeyote bila shida ila kwa asilimia 15 ya akiana mama wajawazito ndio wanajifungua wakiwa wanahitaji msaada wa dharura aidha kuongezewa damu, kufanyiwa upasuaji, au watahitaji huduma ya kitabibu kwa ukaribu na kitalamu amesema Mganga Mkuu wa Mkoa, Dkt. Boniphace Kasululu.
Pamoja na kutokwa kwa damu nyingi wakati wa kujifungua sababu nyingine inayopelekea vifo vingi vya mama mjamzito ni matatizo yanayoambatana na shinikizo la damu yaani kifafa cha mimba, uambukizwa kabla, wakati au baada ya kujifungua, akina mama wanakuja wakiwa na upungufu wa damu kutokana na lishe duni wakati akiwa mjamzito lakini ni sababu ambazo zinaweza kuzuilika shida inabaki kwa watalamu tu kwani kwa wao vyote wamefundishwa hivyo namna ya kuzuia pale yanapotokea, ni swala la watalamu kuwa na nia thabiti ya kuokoa maisha ya mama mjamzito tu.
MWISHO.
2 Nselewa Mkoani RD, 54180 Mlowo-Mbozi
Anuani ya Posta: P.O.BOX 23 SONGWE
Simu: 025 2580305
Simu ya Kiganjani: 025 2580305
Barua pepe: ras@songwe.go.tz
Hakimiliki©2020 Mkoa wa Songwe.Haki Zote Zimehifadhiwa.