WAKULIMA KUPATA MBOLEA YA RUZUKU KWENYE VYAMA VYA USHIRIKA.
SONGWE: Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Mhe. Waziri Kindamba amezindua mpango maalumu wa kugawa mbolea ya Ruzuku kwa wakulima kupitia vyama vya ushirika, wakulima watapata mbolea kupitia vyama vyao vya ushirika vilivyopo kwenye maeneo yao.
Uzinduzi huo umefanyika, Oktoba 21 wakati wa mafunzo kwa ajili ya wenyeviti, makatibu meneja wa vyama vya ushirika, Kwa vyama ambavyo vimepata dhamana ya kuwahudumia wakulima kupata Mbolea ya Ruzuku.
Mhe. Waziri Kindamba amesema Songwe inakuwa ya kwanza Tanzania kuanzisha mpango huu ambao unakwenda kusogeza mbolea ya Ruzuku kwa wakulima waliopo vijijini kupitia ushirika.
"Nampongeza sana Rais wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha shilingi Bilioni 150 kwa ajili ya Mbolea ya Ruzuku na kupunguza kwa bei ya Mbolea kwa 50%, hakika Mama ameupiga mwingi sana" Mhe. Waziri Kindamba Mkuu wa Mkoa wa Songwe.
Mrajis msaidizi wa Ushirika Mkoa wa Songwe, Benjamin Mwangala amesema kwa mujibu ya msingi wa 6 wa Ushirika unataka ushirika kujali jamii kilipo chama cha ushirika, hivyo kupitia mpango huu mwanachama na mwananchi anayeishi karibu na chama anatakiwa kunufaika na Mbolea ya Ruzuku.
Julius Maliki, Afisa mauzo kutoka kampuni ya ETG amesema wameongeza maghala ya kuhifadhia Mbolea ya Ruzuku katika mji wa Vwawa, Mlowo na Tunduma pamoja na usafiri wa kuhakikisha zinafika hadi kwenye vyama vya ushirika.
Mkuu wa Mkoa ametoa wito kwa wakulima kutumia vizuri Mbolea ya Ruzuku ili waweze kulima kwa tija na kuongeza kipato cha mkulima na Taifa.
Pia, Mhe. Waziri Kindamba ametoa wito kwa wakulima kujiunga kwenye vyama vya ushirika ili waweze kupata huduma kwa pamoja.
Wakati huo huo, Mhe. Waziri Kindamba amevitaka vyama ushirika kumiliki mashamba yao na kuanzisha kilimo cha block farming.
MWISHO.
2 Nselewa Mkoani RD, 54180 Mlowo-Mbozi
Anuani ya Posta: P.O.BOX 23 SONGWE
Simu: 025 2580305
Simu ya Kiganjani: 025 2580305
Barua pepe: ras@songwe.go.tz
Hakimiliki©2020 Mkoa wa Songwe.Haki Zote Zimehifadhiwa.