WAKULIMA WATAKIWA KUCHANGAMKIA FURSA YA KIWANDA CHA KUCHAKATA PARACHICHI
SONGWE: Kiwanda cha kuchakata parachichi cha Lima kilichopo wilayani Mbozi kina malengo ya kufikia kuchakata maparachichi tani 100 kwa siku kwa ajili ya kupata mafuta yanayofaa kwa matumzi ya vipodozi kutoka tani 48 ya sasa.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa kampuni ya Lima, Ndg. Tinson Tuloline Nzunda wakati wa ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Songwe alipotembelea kiwandani hapo tarehe 14 Julai 2022 kujionea jinsi kazi zinavyoenda.
Tinson Nzunda amesema tangu kiwanda kianze kufanya kazi Juni 2021 tani 2,700 za matunda ya parachichi zimeishachakatwa na kupata tani 231 za mafuta yanayofaa kwa vipodozi.
“Kampuni kwa sasa tunafunga mitambo mingine mikubwa na lengo letu ni kuweza kuchakata parachichi tani 100 kwa siku na kwa mwaka itakuwa zaidi ya tani 36,000 hivyo wakulima wachangamkie fursa ya kulima parachichi” Tinson Nzunda Mkurugenzi wa Lima.
Pia, Ndg. Nzunda amesema kwa sasa wanalazimika kuagiza maparachichi kutoka Mkoa wa Kagera, Kigoma na Kilimanjaro kwa ajili ya mahitaji ya kiwanda, hii ni kwa sababu maparachichi ni zao la msimu hivyo inapotokea sio msimu wake tunalazimika kwenda kuagiza kwingine ingawa ata ambayo yanakuwepo wakati wa msimu bado hayatoshelezi mahitaji ya kiwanda.
Parachichi la kisasa lina kiwango kikubwa cha mafuta ambayo tunayahitaji tofauti na haya maparachichi ya zamani au ya mbegu ya asili hivyo tunawaimiza wakulima kulima parachichi la mbegu ya kisasa amesema, Ndg. Tinson Nzunda.
Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Mhe. Omary Mgumba amesema uhaba wa parachichi kwenye kiwanda cha Lima ni fursa kubwa sana kwa wananchi wa Songwe kuanza kuwekeza kwenye parachichi kwa kuwa kuna uhakika wa soko.
“Miaka ya nyuma wakulima walianza kukata miti ya maparachichi kwa kuwa walikuwa hawana uhakika wa soko lakini uwepo wa kiwanda cha kuchakata parachichi ndani ya Songwe ni fursa tena kwa wakulima kuanza kuwekeza tena kwani soko lipo na la uhakika” Mhe. Omary Mgumba.
Serikali tumelichukua na tunakwenda kuhamasisha kilimo cha parachichi ambacho itakuwa ni faida kwentu Serikali tutaweza kufanya mambo mawili kwa wakati mmoja, tutatunza mazingira kwa kupanda miti kwa kuwa parachichi ni zao la miti lakini jambo la pili tutaongeza malighafi ya kiwanda hiki.
Kwa upande Mkuu wa wilaya ya Mbozi, Mhe. Cosmas Nshenye amemshukuru mkurugenzi wa Lima Ndg. Tinson Nzunda kwa kuwekeza nyumbani kwao na kutengeneza ajira za kutosha.
Wakati huo huo Mkuu wa Mkoa amesema Serikali inaendelea kuimarisha upatikanaji wa umeme ambao hautakuwa changamoto kwa wawekezaji wa viwanda, kituo kikubwa kinajengwa Tunduma cha zaidi ya KV 440 ambacho kikikamilika kitatatua changamoto ya upungufu wa umeme kwenye viwanda vya Mkoa wa Songwe.
MWISHO.
2 Nselewa Mkoani RD, 54180 Mlowo-Mbozi
Anuani ya Posta: P.O.BOX 23 SONGWE
Simu: 025 2580305
Simu ya Kiganjani: 025 2580305
Barua pepe: ras@songwe.go.tz
Hakimiliki©2020 Mkoa wa Songwe.Haki Zote Zimehifadhiwa.