Wananchi 13,476 wa kata ya Kapele yenye vijiji nane na vitongoji 39 Wilayani Momba, wanatarajia kupata huduma za upasuaji ikiwemo upasuaji wa dharura kwa akina mama wajawazito kufuatia kuanza kwa ujenzi wa kituo cha Afya katika kata hiyo.
Wananchi hao waliojitokeza kwa wingi na kujitolea nguvu kazi kwa kusafisha eneo la ujenzi na kuchimba msingi wamesema, kukosekana kwa kituo cha Afya katika kata hiyo kulipelekea wao kufuata huduma za upasuaji takribani kilomita 106 huku miundombinu ya barabara ikiwa mibovu.
Wamesema wanaishukuru serikali kwa kutoa shilingi milioni 400 kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho kinachotarajiwa kukamilika ifikapo Disemba 2018 na hivyo kuwapunguzia gharama za usafiri wa kufuata huduma hizo mbali.
Afisa Mtendaji wa Kata ya Kapele Erasto Simchimba amesema kazi zilizokwisha fanyika katika eneo la ujenzi ni upimaji wa eneo hilo la ekari 25, kukusanya mawe na mchanga na uagizaji wa vifaa vya ujenzi huku hamasa ya wananchi kujitolea ikiwa ni kubwa.
Simchimba amesema, “wananchi wamehamasika kujitolea kwakuwa wanafahamu umuhimu wa kituo hiki na tayari wamefyeka miti na kusawazisha eneo hili na sasa wanachimba msingi wa majengo matano ambayo ni jengo la wagonjwa wa nje, jengo la wagonjwa wa ndani, chumba cha upasuaji, maabara na jengo la wazazi”.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brigedia Jenerali Nicodemus E Mwangela ametembelea eneo la ujenzi wa Kituo cha Afya Kapele na kushiriki pamoja na wananchi shughuli ya uchimbaji wa msingi wa kituo hicho.
Brig. Jen. Mwangela amewasisitiza wananchi kuendelea na moyo huo wa kujitolea kwakuwa kituo hicho cha afya kitawanufaisha wao huku akiwasisitiza kutunza miundombinu ya kituo hicho mara kitakapokamilika.
Aidha kuhusu ubovu wa barabara ya Kakozi-Ilonga yenye urefu wa Kilomita 50 amewaeleza wananchi hao kuwa anawapongeza Wakala wa Barabara Vijijini katika Halmashauri ya Wilaya ya Momba kwa kutenga shilingi milioni 300 ambazo zitaanza matengenezo kwa kilomita 18 za barabara hiyo.
Wakati huo Brig. Jen. Mwangela amewataka wananchi wa kata ya Kapela ambayo iko mpakani na nchi jirani ya Zambia kuchukua tahadhari ya ugonjwa ebola na kutoa taarifa katika zahanati iliyopo katika kata hiyo mara watakapomuhisi mtu mwenye dalili za ugonjwa huo.
Ameongeza kuwa kata ya Kapele iko mpakani na kumekuwa na mwingiliano na nchi jirani ya Zambia kutokana na mahusiano mazuri hivyo kuwa katika hatari ya kupata ugonjwa huo kutoka kwa raia wa Congo wanaopitia Zambia aidha amewasihi kudumisha mahusiano mazuri kwa kutii sheria za nchi jhiyo wanapokuwa huko.
2 Nselewa Mkoani RD, 54180 Mlowo-Mbozi
Anuani ya Posta: P.O.BOX 23 SONGWE
Simu: 025 2580305
Simu ya Kiganjani: 025 2580305
Barua pepe: ras@songwe.go.tz
Hakimiliki©2020 Mkoa wa Songwe.Haki Zote Zimehifadhiwa.