Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brig.Jen. (Mst) Nicodemus E Mwangela amefanya ziara ya kukagua utekelezaji wa Mpango wa TASAF katika Wilaya za Momba na Ileje ambapo amesema ameridhishwa na namna ambavyo wanufaika wa mpango huo wameweza kupiga hatua katika kujikwamua kutoka katika umasikini.
Brig.Jen. (Mst) Mwangela amewashauri wanufaika hao kuendelea kuwekeza katika elimu na afya kwani ndio msingi mkubwa wa kujiondoa kwenye umasikini.
"Ndugu zangu hakuna mtu aliyezaliwa ili awe masikini, wote tunaweza kutoka kwenye umasikini endapo tutahakikisha tunawasimamia watoto wetu walioko kwenye mpango wa TASAF wapate elimu pia tuwekeze katika afya hasa kwenye mfuko wa afya ya jamii ili tuweze kupata huduma za afya", Brig.Jen. (Mst) Mwangela.
Brig.Jen. (Mst) Mwangela pia amewasisitiza kutowakatisha masomo watoto walioko kwenye mpango wa TASAF kwa kuwaozesha mapema bali wawasimamie watoto hao hususan wa kike wasome mpaka watakapo hitimu ili waweze kuwakomboa wazazi wao na wajikomboe wenyewe kutoka katika umasikini.
Ameongeza kuwa lengo la mfuko wa TASAF ni kumsaidia mnufaika apige hatua haraka kutoka kwenye umasikini na aweze kuyamudu maisha ya kaya yake kwa kuwa na uhakika wa chakula, huduma za fya na elimu na hata kuchangia katika pato la Taifa kwa kuzalisha mali kupitia kilimo, ufugaji na biashara.
Jakson Mwabeza mmoja wa wanufaika kutoa Wilaya ya Ileje kijiji cha Ilulu amesema kabla ya kuingia katika mpango wa TASAF maisha yake yalikuwa duni lakini baada ya mpango huo ameweza kujenga nyumba ya bati, amenunua baiskeli 14 na ana uhakika wa chakula nyumbani.
"Wakati mkutano wa kijiji umeitishwa ili kuwapata walengwa wa TASAF nilionekana mimi pia ni mmoja wapo wa walengwa ila niliona kama udhalilishaji kutokana na hali yangu ya umasikini, nashukuru mtendaji wa kijiji kwa kunielewesha kuhusu mpango huu, hadi sasa mafanikio niliyo nayo yametokana na mpango wa TASAF", amesema Mwabeza.
2 Nselewa Mkoani RD, 54180 Mlowo-Mbozi
Anuani ya Posta: P.O.BOX 23 SONGWE
Simu: 025 2580305
Simu ya Kiganjani: 025 2580305
Barua pepe: ras@songwe.go.tz
Hakimiliki©2020 Mkoa wa Songwe.Haki Zote Zimehifadhiwa.