Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe Exaud Kigahe, amefanya Ziara tarehe 9 Agosti 2023 katika Mkoa wa Songwe na kupokelewa na mwenyeji wake Mkuu wa Mkoa wa Songwe Dkt Francis Michael. Ziara hiyo ilijumuisha Kaimu Meneja wa Shirika la Maendeleo la Viwanda Vidogo (SIDO) Mbeya, Bi Sari Magarasi, pamoja na wadau wengine wa Biashara na Viwanda.
Ziara hiyo ilikuwa ni fursa adhimu ya kuwaleta pamoja viongozi na wataalamu wa sekta ya viwanda na biashara ili kujadili njia bora za kukuza uchumi. Ziara hiyo ililenga kujadili mbinu za kuongeza ufanisi katika uzalishaji, kukuza thamani ya bidhaa zinazozalishwa, na kuhamasisha uwekezaji katika mkoa huo. Pia, walijadili jinsi ya kukabiliana na changamoto za kiuchumi kama vile upatikanaji wa masoko, na hata na changamoto zinazo kabili sekta binafsi katika uwekezaji.
"Nipo hapa kwaajili ya mpango wa kuboresha mazingira ya sekta binafsi ambayo ni maelekezo ya Rais Samia kuboresha sekta binafsi ambayo ni injini ya uchumi wa Tanzania na Dunia kwa ujumla Ujue sekta binafsi ikisimamiwa vizuri inafanya vizuri.Tunataka kuona taasisi za Serikali zinawezesha taasisi binafsi kupata huduma bila vikwazo ili kurahisisha ufanyikaji wa biashara katika mpaka wa Tunduma".
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Dkt Francis Michael amesema kuwa Songwe ni mkoa wa kimkakati na wamejipanga kuwaita wawekezaji kuwekeza zaidi katika sekta ya viwanda vitakavyozalisha mchele kutokana na mkoa huo kuzalisha mchele bora na usiotumia mbolea. aidha amewataka Sido kujenga ofisi yao karibu na ofisi za makao makuu ya mkoa wa Songwe ili kurahisisha wananchi kupata huduma jirani.
kaimu Meneja wa SIDO Mbeya, Bi Sari Magarasi,alitoa ufafanuzi kuhusu jukumu la SIDO katika kuendeleza viwanda vidogo vidogo. Alielezea jinsi SIDO inavyotoa mafunzo na ushauri kwa wajasiriamali ili kuwawezesha kuanzisha na kuendeleza viwanda vidogo vinavyotengeneza bidhaa mbalimbali. Hii ina lengo la kukuza uchumi wa eneo hilo na kutoa fursa za ajira.
Ziara hiyo pia inaonyesha dhamira thabiti ya serikali katika kufanya kazi kwa karibu na viongozi wa ngazi za chini na wadau wa sekta ya viwanda ili kufikia malengo ya maendeleo. Kwa kuwekeza katika viwanda vidogo vidogo na kusaidia wajasiriamali, Mkoa wa Songwe una nafasi nzuri ya kustawi kiuchumi na kuleta mabadiliko chanya kwa wananchi wake.
MWISHO.
2 Nselewa Mkoani RD, 54180 Mlowo-Mbozi
Anuani ya Posta: P.O.BOX 23 SONGWE
Simu: 025 2580305
Simu ya Kiganjani: 025 2580305
Barua pepe: ras@songwe.go.tz
Hakimiliki©2020 Mkoa wa Songwe.Haki Zote Zimehifadhiwa.