Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu(katikati),Mkuu wa mkoa wa Songwe Mhe. Dkt Francis Michael (Upande wa kushoto),Waziri wa Afya, Mhe. Ummy Mwalimu akiwa Mkoa wa Songwe ametoa wito kwa Wananchi wa mikoa sita iliyopo mipakani nchini Tanzania, ambayo ipo kwenye hatari ya kuwa na maambukizi ya ugonjwa wa Polio, kuwapeleka watoto wenye umri chini ya miaka nane kupata chanjo ya pili ya ugonjwa wa Polio. Hii ni baada ya mtoto mmoja kubainika na ugonjwa huo wilayani Sumbawanga, mkoani Rukwa.
Waziri Ummy alitoa taarifa hii wakati wa ziara yake ya siku tatu mkoani Songwe, ambapo alikagua huduma za afya katika Hospitali ya Wilaya, vituo vya afya, na zahanati, pamoja na kuongea na Wananchi katika Kata za Mbuyuni, Chang'ombe, na Mkwajuni wilayani Songwe. Ameeleza kuwa chanjo ya Polio kirusi cha pili itaanza kutolewa tarehe 21 Septemba 2023 katika mikoa iliyopo mpakani.
Waziri Ummy amewasihi Wananchi kujitokeza kwa wingi kupeleka watoto wao kupata chanjo, huku akitangaza lengo la kuwafikia zaidi ya milioni 3 ya watoto wote wenye umri chini ya miaka nane katika mikoa hiyo sita. Kwa mfano, mkoa wa Songwe pekee unatarajia kuwapa chanjo takribani watoto 400,000.
Mikoa hiyo sita iliyopo mipakani ambayo inapewa kipaumbele katika kampeni ya chanjo ya Polio kirusi cha pili ni Songwe, Rukwa, Katavi, Mbeya, Kigoma, na Kagera, ambayo inapakana na nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Malawi, na Burundi, ambazo zimeripotiwa kuwa na visa vya wagonjwa wa Polio kirusi cha pili.
Licha ya Tanzania kupata cheti kutoka Shirika la Afya Duniani mwaka 2015 kwa kutangazwa kuwa haina maambukizi ya Polio, mwaka 2023 kulitokea kisa cha mtoto mwenye Polio kirusi cha pili katika Manispaa ya Sumbawanga mkoani Rukwa, hivyo kuonyesha umuhimu wa kampeni hii ya chanjo.
Mkuu wa Wilaya ya Songwe, Solomon Itunda, ameeleza kuwa baada ya kupokea maelekezo kutoka Wizara ya Afya, wameanza kutoa elimu kwa Wananchi katika Kata zote kuhusu maandalizi ya chanjo hii. Wanahamasisha Wananchi kujitokeza kwa wingi kuanzia tarehe 21 Septemba kuwapeleka watoto wao kwenye vituo vya afya na zahanati kwa ajili ya kupata chanjo. Pia, wameandaa vipeperushi vinavyoelezea umuhimu wa chanjo ya Polio.
Mama Janet Frenk, mkazi wa Kata ya Mbuyuni wilayani Songwe, ameeleza kuwa baada ya kupata elimu kupitia ziara ya Waziri wa Afya, atajitahidi kuhakikisha mwanae mwenye umri wa miaka miwili anapata chanjo hiyo muhimu. Ameeleza kuwa baadhi ya akina mama wanaweza kusita kupata chanjo kwa watoto wao kutokana na umbali wa vituo vya afya na zahanati katika Wilaya hiyo.
MWISHO.
2 Nselewa Mkoani RD, 54180 Mlowo-Mbozi
Anuani ya Posta: P.O.BOX 23 SONGWE
Simu: 025 2580305
Simu ya Kiganjani: 025 2580305
Barua pepe: ras@songwe.go.tz
Hakimiliki©2020 Mkoa wa Songwe.Haki Zote Zimehifadhiwa.